Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Monday, October 27, 2014

NECTA YAFANIKIWA KUDHIBITI UDANGANYIFU NA WIZI WA MITIHANI YA TAIFA NCHINI


 Mkuu wa Idara ya Fedha na Utawala wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) Bw. Daniel Mafie akiwaeleza waandishi wa habari leo jijini Dar s salaam kuhusu utaratibu wa kutoa nakala za vyeti kwa watahimiwa waliopoteza vyeti vyao ambapo utaratibu huo unahusisha uchunguzi wa uhalali wa mwombaji.  Kulia ni Afisa Habari wa NECTA John Nchimbi na kushoto ni Msaidizi wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania Bi Glee Magemba.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia mkutano wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) na Vyombo vya habari uliofanyika leo jijini Dar es salaam ukilenga  kuonyesha mafanikio ya Baraza hilo nchini.
**************************************
Frank- Mvungi - MAELEZO
Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limedhibiti na kuondoa kabisa tatizo la wizi wa Mitihani ya Taifa na udanganyifu wakati wa Mitihani katika ngazi mbalimbali za elimu nchini.

Mafanikio hayo yametokana na ushirikiano uliopo kati ya NECTA na kamati za uendeshaji mitihani katika ngazi za mikoa na wilaya ili kutatua tatizo la wizi wa mitihani ya taifa na udanganyifu wakati wa mitihani uliokuwa ukifanywa kinyume na taratibu za baraza la mitihani.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Idara ya Fedha na Utawala wa Baraza hilo Bw. Daniel Mafie wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Jjijini Dar es salaam uliolenga kueleza mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa.

Akifafanunua Mafie amesema kuwa katika mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi mwaka 2013 watahimiwa waliofutiwa matokeo kwa kufanya udanganyifu walikuwa 13 tu ikilinganishwa na watahiniwa 9,736 waliobainika kufanya udanganyifu mwaka 2011.

Aidha Mafie aliongeza kuwa katika Mtihani wa Kidato cha nne mwaka 2013 watahimiwa waliofutiwa matokeo kwa kufanya udanganyifu walikuwa 272 ikilinganishwa na watahimiwa 789 mwaka 2012 na 3,303 mwaka 2011.

Akieleza zaidi kuhusu mafanikio yaliyofikiwa Mafie alisema Baraza hilo limeweza kusanifu mifumo ya Kompyuta yenye uwezo wa kupanga shule katika makundi ya ubora wa ufaulu katika matokeo ya mitihani ya Taifa.

Katika kukabiliana na tatizo la watu wanaotumia vyeti vya watu wengine au kughushi vyeti wakati wa kuomba ajira au nafasi za masomo katika shule mbalimbali ambapo kuanzia mwaka 2008/2009 Baraza hilo lilianzisha utaratibu wa kuweka picha za watahimiwa katika vyeti vyao.

Katika utaratibu huo vyeti hivyo viliwekewa alama za kiusalam hali ambayo imesaidia Baraza hilo kuwa na uwezo wa kubaini kwa haraka na kuwachukulia hatua wale wanaoghushi vyeti au kutumia vyeti vya watu wengine.

Baraza la Mitihani la Tanzania ni Taasisi ya Umma iliyochini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliyoanzishwa kwa sheria ya Bunge Namba 21 ya mwaka 1973 na marekebisho yake ya mwaka 1998 na 2002 kwa ajili  ya kuendesha mitihani ya Taifa kwa lengo la kuweka misingi ya sera ya mitihani, kuendesha mitihani na kutunuku stashahada mbalimbali na vyeti kwa watahiniwa wanaofuzu na kufaulu mitihani iliyo chini yake kisheria.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...